Serikali yatangaza kupandisha bei ya vinywaji baridi, bia na mvinyo kutoka nje.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyasema hayo, wakati akisoma Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 bungeni mjini Dodoma.
“Napendekeza kufanya marekebisho kwenye sheria ya ushuru wa bidhaa, sura 147 kama ifuatavyo: Hata hivyo, kwa kuzingatia mkakati wa Taifa wa kukuza uchumi wa viwanda, baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini hazitafanyiwa marekebisho hayo. Mabadiliko ninayopendekeza ni kama ifuatavyo:-
“Ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji baridi kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita,ushuru wa bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka nje kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita. Aidha, Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 58 kwa lita.”
Aidha ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini (local juices) utashuka kutoka shilingi 9.5 kwa lita na kuwa shilingi 9.0 kwa lita,Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini (imported juices) kutoka shilingi 210 kwa lita hadi shilingi 221 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 11 kwa lita.
Hata hivyo,ushuru wa bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (Beer from Local Unmalted Cereals) kutoka shilingi 429 kwa lita hadi shilingi 450 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 21 kwa lita,Ushuru wa Bidhaa kwenye bia nyingine zote kutoka shilingi 729 kwa lita hadi shilingi 765 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 36 kwa lita.
“Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka shilingi 534 kwa lita hadi shilingi 561 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 27 kwa lita,Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utashuka kutoka shilingi 202 kwa lita na kuwa shilingi 200 kwa lita;
Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 2,236 kwa lita hadi shilingi 2,349 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 113 kwa lita.”
Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje kutoka shilingi 3,315 kwa lita hadi shilingi 3,481 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 166 kwa lita. Aidha,ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 3, 315 kwa lita.”
No comments:
Post a Comment