FUNZO KWA MAKOCHA WA VILABU VINGINE KWA UBINGWA WA REAL MADRID - JONGOTZMEDIA.COM

Latest

efm

">">WHATSAPP NUMBER 0757357341

Pages

Sunday, 4 June 2017

FUNZO KWA MAKOCHA WA VILABU VINGINE KWA UBINGWA WA REAL MADRID

Real Madrid imeweka historia ya kutetea ubingwa wa michuano ya klabu bingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League ambapo klabu ya mwisho kuweza kutetea ubingwa wa kombe hilo ilikuwa ni AC Milan mwaka 1990
Sambamba na kutetea ubingwa, ni lazima tukumbushane kuwa huku wakali hao wa Santiago Bernabeu ndio wanashikilia rekodi ya kutwaa taji hilo mara nyingi zaidi (12) kwenye historia ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya vilabu barani Ulaya.
Mabao manne ya Real Madrid kutoka kwa Cristiano Ronaldo (2), Casemiro na Asensio yalitosha kabisa kulifunika bao maridadi la Mario Mandzukic wa Juventus na kunyakua ubingwa kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye dimba la Millenium jijini Cardiff huko nchini Wales.
Kunako usiku wa fainali hiyo ya UEFA, watu mashuhuri duniani katika tasnia ya soka waliweza kukusanyika kwenye dimba la Millenium ili kushuhudia kwa macho yao jinsi ambavyo makocha Zinadine Zidane na Massimiliano Allegri wakitambiana.
Sio ajabu kuona wanamuziki mashuhuri, waigizaji waliotukuka sambamba na makocha wakubwa duniani wakiwepo majukwaani kutazama mtanange huu ambao hata mimi ningekuwepo jijini Cardiff nisingekubali unipite.
Licha ya kutazama mpira dakika 90 na kushindwa kuiona japo sura yake tu, lakini naamini fika mtu kama Antonio Conte asingeweza kukosa kuwepo dimbani Millenium kuiunga mkono timu yake kipenzi ya Juventus ambayo aliweza kuipa mafanikio kama mchezaji lakini pia kama kocha.
Image result for antonio Conte winning epl
Kocha wa Chelsea, Antonio Conte
Antonio Conte ambaye ametoka kuipa Chelsea ubingwa wa Uingereza wiki kadhaa zilizopita alikuwa na kila sababu ya kuwepo uwanjani hapo kutazama mechi hiyo ukizingatia kuwa London sio mbali na Cardiff, lakini pia mapenzi yake kwa Juventus ndio yalikuwa sababu kubwa zaidi kwani hata angekuwa jijini Roma bado angekwea pipa tu.
Unaweza kujiuliza kwanini nimzungumzie Conte tu wakati makocha wengi walikuwepo uwanjani hapo kushuhudia mechi hiyo ya kusisimua, lakini nna kila sababu ya kufanya hivyo.
Conte amesajiliwa Chelsea msimu uliopita na katika msimu wake wa kwanza ameweza kuipa Chelsea ubingwa wa ligi. Msimu uliopita Chelsea ilikuwa ikipumulia mashine na kumaliza katika nafasi ya kumi na ujio wa Conte ulikuwa na maana ya kuirudisha timu hiyo kwenye Top 4 tu ili iweze kucheza michuano ya UEFA msimu unaofata.
Kwa bahati nzuri Conte ameweza kuvuka malengo kutoka kwenye kurudi Top 4 hadi kuchukua ubingwa kabisa. Chelsea sasa imerudi UEFA sio kwa kumaliza katika top 4 tu, bali inaingia ikiwa kama bingwa wa Uingereza, kwahiyo unaweza ukaona uzito wa kumzungumzia Conte na Chelsea yake kwa wakati huu.
Conte aliambatana na ndugu yake Gianluigi Conte ambaye pia ni mmoja wa makocha kwenye benchi la ufundi la Chelsea kuishuhudia Juve ikimenyana na Real Madrid na bila shaka wawili hao watakuwa wameyaona yaliyojiri. Najua ilikuwa ni siku mbaya sana kwa ndugu hao wawili, lakini lazima kuna kitu wametoka nacho uwanjani hapo.
Wakati naiangalia Madrid ikiisasambua Juventus kwa mirindimo ya kila namna, kwa mbali nilikuwa namuwaza Antonio Conte na Chelsea yake ambayo na yenyewe imeweza kuvisasambua vilabu vya Uingereza msimu huu.
Namuangalia Conte kwa jicho la tatu na najaribu kuwaza nini ambacho kocha huyo muitaliano atakuwa ameondoka nacho uwanjani hapo lakini kuna vitu nahisi mimi na yeye tumewaza sawa.
Safu ya Kiungo
Conte bila shaka atakuwa ameiona safu ya kiungo ya Real Madrid ambayo bila kupepesa kope nathubutu kusema kuwa ndio imeiua Juventus leo hususani kipindi cha pili.
Kwenye safu hiyo ya kiungo ya Madrid, Conte atakuwa amemuona Modric anavyozunguka uwanja mzima kama askari wa doria katika harakati za kuhakikisha waharifu wa Juve wanatulizwa. Katika kumuona Modric, najua Conte atakuwa amemfananisha na Ngolo Kante ambaye msimu huu naye amekuwa hashikiki, hivyo kwa hapo Conte hajaona wivu sana.
Wakati akihisi kuwa na yeye anaye Modric kwenye kikosi chake cha Chelsea, Conte pia atakuwa amewaona Toni Kroos na Casemiro walivyokuwa wakifanya shughuli pevu pale katikati na bila shaka atakuwa amejiuliza, Je, Cesc Fabregas, Nemanja Matic au Nathan Chalobah wanaweza kufanya shughuli waliyoifanya kina Kroos? Mimi sijui.
Ronaldo
Wakati Conte akishuhudia miujiza ya jini Modric ambaye alikuwepo kila kona ya uwanja, bila shaka atakuwa alikuwa akimuangalia Cristiano Ronaldo kwa jicho la sitaki nataka. Conte alimuona Ronaldo mwenye njaa ya kufunga, Ronaldo mwenye uchu wa kufanya jambo ili Madrid yake iweze kuneemeka.
Image result for Ronaldo vs juventus
Mshambuliaji wa Real Madri, Cristiano Ronaldo
Bila shaka akili ya Conte kwa haraka haraka ikamuwaza Diego Costa, halafu papo hapo ikajiuliza je, Costa ana njaa ya kufunga kama ya Ronaldo? Je, Costa anaweza kuwa na uchu wa kuibeba Chelsea kwenye michuano ya UEFA msimu ujao kama Ronaldo ninayemuona sasa? Bila shaka akili yake ilikosa kumpa majibu sahihi ingawa ukweli anaujua mwenyewe.
Marcelo, Dani Alves, Carvajal
Kadri dakika zilivyokuwa zikizidi kwenda, macho ya Conte yalikuwa hayapumziki yakiangalia huku na huko, kwani licha ya kumuona Modric kila kona ya uwanja, bado pia aliweza kuwaona vizuri kina Marcelo, Dani Alves na Carvajal jinsi ambavyo walikuwa wakipanda na kusababisha mashambulizi licha ya wao kuwa ni mabeki.
Kwa haraka haraka akili ya Conte ikamuwaza Victor Moses na Marcos Alonso kwenye Chelsea yake huku akijiuliza je, msimu ujao Moses na Alonso wataweza kufanya mambo yale ayaonayo kutoka kwa Marcelo na viberenge wenzie? Kadri muda ulivyozidi kwenda, nna uhakika kichwa cha Conte kilianza kupata mawazo zaidi.
Somo muhimu
Kwa kifupi nnachotaka kusema ni kuwa Conte akiwa ni miongoni mwa makocha watazamaji waliohudhuria fainali hii atakuwa amejifunza mengi hususani juu ya nini michuano mikubwa kama ya UEFA inataka.
Conte ameweza kuipa Chelsea ubingwa wa ligi ya Uingereza na sasa anaingia kwenye kinyang’anyiro cha UEFA huku fainali ya Cardiff ikimpa picha nzima.
Kwanza kabisa ameona jinsi ambavyo timu kama Real Madrid ina kikosi kikubwa. Licha ya kujaza wachezaji hatari ndani, lakini benchi lao lina wachezaji hatari pia kiasi kwamba huoni afadhali ya aliyeingia kutokea benchi.
Benchi lina watu kama Bale, Morata, Asensio, Nacho, Pepe, James Rodriguez na wengine lukuki wenye majina makubwa hali ambayo inadhihirisha kuwa Madrid sio timu ya mchezo mchezo na imestahili kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo.
Kwa kuliona hilo, Conte arudi kwenye kikosi chake atazame kuwa akishawapanga kina Kante, Hazard, Luiz na Costa ndani, nje anabaki nani huko benchi? Je, Costa akiumia kuna mtu kama yeye nje? Swali linaanzia hapo.
Wakati Benzema akiwa ndani, Morata yupo benchi halafu ukiuliza utaambiwa ndio Madrid hiyo hiyo inayomtaka Kylian Mbape au Erick Aubameyang, lakini kwa Conte mbadala wa Costa ni Michy Batshuayi ambaye bado sio mtu wa kumtegemea aje kukubadilishia matokeo. Nafikiri hilo Conte ameliona pia.
Kuna mengi ya kuzungumza, lakini Conte hana budi kuichukulia jeuri hii ya Madrid kama somo kwake na sio kuishia kumfuta machozi Gigi Buffon kwa kipigo kizito alichopokea.
Conte lazima aelewe Chelsea ina kikosi kidogo sana ambacho baadhi ya wachezaji wakiumia basi mashabiki roho mkononi
Conte lazima aelewe kuwa huko kwenye UEFA ambako alikuwa anakutamani ni kugumu na kunahitaji wachezaji wenye uwezo unaojibeba wenyewe kabla ya kubebwa na timu.
Conte lazima aelewe kuwa kabla ya kushona suti kali ya kuvaa kwenye mechi za UEFA ni lazima awe na wachezaji kaliba ya Marcelo, Ronaldo, Modric na wengineo ambao wanaweza kufanya miujiza muda wowote wa mchezo na sio kuishia kutegemea uwezo wa Eden Hazard pekee ambaye kuna muda unaweza kuhisi kama safu ya ushambuliaji imemsusia yeye pekee huku Costa akiwa ‘busy’ kuwaadabisha mabeki wanaomkaba.
Conte lazima aelewa kuwa UEFA ni ngumu, asipoingia sokoni kuziwinda saini za kina Marco Veratti, Raja Nainngolan, Morata, Van de Vidjki na wengine wa aina hiyo, basi maisha yake yatakuwa magumu sana kwa kutegemea kikosi kidogo alichonacho kifanye miujiza ilichofanya msimu huu.
Sio tu kwa Conte, bali timu zote za Uingereza ambazo zinawania kurudisha heshima kwenye michuano ya UEFA msimu ujao zijifunze kutoka kwa Zidane na Madrid yake juu ya nini michuano hiyo inataka na sio kuishia kutuaminisha kwa mdomo kuwa ligi ya Uingereza ndio ligi ngumu zaidi duniani badala ya kuthibitisha kwa vitendo, Tukutane msimu ujao!!!.

No comments:

Post a Comment