Klabu ya soka ya Singida United iliyopanda ligi kuu msimu huu imeanza mazoezi makali uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam kwa maandalizi ya michuano ya SportPesa Super League itakayorindima nchini kuanzia Juni 5.
Kampuni ya kamari ya SportPesa toka nchini Kenya wadhamini wakuu wa vilabu vya Tusker FC , AFC Leopards, Nakuru all stars zote toka Kenya na wakongwe wa soka nchini Yanga SC , Simba SC na wageni hawa wa ligi kuu Singida United, wameanzisha michuano maalumu kwa ajili ya timu wanazozipa udhamini ili kuboresha michezo ukanda wa Afrika mashariki itakayopigwa katika dimba la Uhuru na mshindi kujinyakulia milioni 60.
Singida ambao wanajipanga vyema kwa msimu mpya wa ligi kuu 2017-18 ikiwa ni mara yao ya kwanza tayari wameanza mazoezi katika uwanja wa Uhuru jijini Dar na wakitamba kuitumia michuano hiyo kujitathimini uwezo wao baada ya kufanya usajili mzuri ndani na nje ya nchi.
Tayari wachezaji wao toka nje ya nchi wamewasili nchini kwa ajili ya michuano hiyo ambayo wao wanaipa umuhimu kubwa kujenga umoja kitimu na masuala mengine ya kiufundi.
Mwalimu mkuu wa timu hiyo bwana Hans Van Pluijm ambaye aliwika vyema na mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara , amesema ataitumia michuano hiyo kuwatizama vijana wake ambao kwa asilimia 80 ni kikosi kipya na baada ya hapo wataingia kwenye kambi maalumu ndani au nje ya nchi kwa ajili ya kukisuka kikosi chake kiwe cha ushindani ligi kuu.
” mara nyingi timu ambazo zinapanda ligi kuu kwa mara ya kwanza, msimu wao wa kwanza hulenga kubakia ligi kuu na sio kutwaa ubingwa lakini nawaandaa vijana wangu kutwaa ubingwa wa ligi kuu na kombe la ASFC . Naijua vyema ligi ya hapa kikubwa wasimamizi wa ligi wazingatie kanuni na sheria kwa vilabu vyote” alieleza kocha huyo .
No comments:
Post a Comment